KLABU ya Simba imeshindwa kuwafungulisha zawadi za Boxing day mashabiki wake baada ya jioni hii kufungwa na Kagera Sugar
KLABU ya Simba imeshindwa kuwafungulisha zawadi za Boxing day mashabiki wake baada ya jioni hii kufungwa bao 1-0 na Kagera Sugar ukiwa ni mchezo wa raundi ya nane wa Ligi ya Vodacom Tanzania bara uliochezwa kwenye uwanja wa taifa Dar es Salaam.
Kagera Sugar inayojulikana kama kiboko ya timu vigogo baada ya kuifunga Yanga kwenye mchezo wa raundi ya tano msimu huu waliingia katika mchezo huo kwa ari kubwa na kuonyesha kiwango cha juu huku wakishangiliwa na mashabiki wa Yanga ambao wanaupinzani mkubwa na Simba.

Hiyo ni mechi ya kwanza Simba kupoteza msimu huu huku ikiwa na nyota wake wate iliyowasajili kwenye dirisha dogo ambao ni Danny Sserunkuma Simon Sserunkuma na Jjuku Murshid nakufanya timu hiyo ibakiwe na pointi zake tisa huku ikiwa imeshinda mchezo mmoja kutoka sare sita na kufungwa mchezo mmoja.
Simba iliyoingia na matuaini makubwa ya kupata ushindi wa pili baada ya kuwafunga watani zao Yanga wiki mbili zilizopita kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe , Simba ilijikuta ikishindwa kufurukuta nyumbani.
Kagera ilipata bao lake latika dakika ya 10 ya mchezo likifungwa na Atupele Green aliyefunga kwa kichwa baada ya kipa wa Simba Ivo Mapunda kushindwa kudaka mpira wa kurusha na kumkuta mfungaji aliruka kichwa na mpira kujaa wavuni.
Kabla ya bao hilo, Simba ndio waliouanza kwa kasi mchezo na kupoteza nafasi nyingi kupitia kwa Danny Sserunkuma dakika ya tano baada ya shuti lake kudakwa na kipa wa Kagera, Agaton Anthon.
Emmanuel Okwi pia alikosa bao katika dakika ya 8 baada ya shuti lake kutoka nje na dakika mbili baadaye Simon Sserunkuma alikosa bao lingine baada ya shuti lake kupaa juu ya lango.
Mwishoni mwa kipindi cha kwanza, Simba ilicharuka zaidi lakini haikusaidia kwani matokeo yalibaki hivyo mpaka mapumziko.
Simba ilianza kipindi cha pili na mabadiliko ambapo kocha wake Patrick Phiri alimtoa Ramadhani Singano na kumuingiza Elius Maguli.
Aidha katika dakika ya 55 Simba ilifanya mabadiliko mengine kwa kumtoa Awadhi Juma na nafasi yake kuchukuliwa na Shaaban Kisiga, dakika hizo Simba ilizidisha mashambulizi na kufika langoni mwa Kagera mara kwa mara.
Kuanzia dakika ya 60 Kagera walibadilika na kutawala mchezo huku wakipoteza nafasi ya kufunga na hapo ndipo Simba walipomtoa Danny Sserunkuma na nafasi yake kuchukuliwa na Saidi Ndemla huku Kagera wakimtoa Benjamin Asukile na kuingia Victor Hussein.
Kwa ujumla katika mechi hiyo, Danny Sserunkuma ameonesha kiwango cha kawaida na katika muda aliocheza amepoteza nafasi tatu za wazi.
Matokeo hayo yameifanya Kagera Sugar kusogea kwenye msimamo mpaka nafasi ya nne baada ya kufikisha pointi 13, Simba ikibaki nafasi ya nane na pointi zake tisa.
No comments:
Post a Comment